Askofu mkuu Ruwaichi ateuliwa kuwa Askofu mwandamizi mrithi, Dar

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

*Askofu mkuu Ruwaichi ateuliwa kuwa Askofu mwandamizi mrithi, Dar!*

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi ameteuliwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam.

21/06/2018 12:01



Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Ruwaichi alizaliwa tarehe 30 Januari 1954, Mulo, Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 25 Novemba 1981. Tarehe 9 Februari 1999 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu na kuwekwa wakfu tarehe 16 Mei 1999.

Tarehe 15 Januari 2005, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na kusimikwa rasmi tarehe 19 Februari 2005. Tarehe 10 Novemba 2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza na kusimikwa rasmi tarehe 9 Januari 2011. Leo hii, ameteuliwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!



No comments